Tuzungumze kuhusu swala zima la kudhibiti taka katika nyumba zetu za kuishi bila kujali ni ya kwako au ni ya kupanga. Kwanza, maana ya takataka ni kitu au vitu ambavyo havifai tena, havitumiki tena, si vya muhimu tena. Japo hiyo tafsiri haijakamilika vizuri.

Tafsiri nyingine inasema kwamba, takataka ni vitu ambavyo kwa muda huo si vya muhimu tena baada ya mtumiaji wa muda huo kutokuwa na matumizi navyo tena, hivyo hutaka kuvitupa au tayari ameshavitupa! Ni vitu ambavyo aliyenavyo yupo katika maamuzi ya kuvitupa au hutaka kuvitupa. Vitu hivi huwa vimetoka kutumika katika uzalishaji, ubadilishaji au ulaji.

Aina ya taka huweza kugawanywa kutokana na namna mbalimbali za uchambuzi. Huweza kugawanywa katika hali zake za kiumbo kama vile taka-maji na taka-ngumu. Pia huweza kugawanywa kutokana na mifumo ya uzalishaji na athari zake; mfano taka za hospitali, majumbani, za kikemikali, viwandani n.k.

Maana ya kudhibiti taka ni hatua na michakato yote inayopaswa kufanywa tangu hatua ya awali kabisa ya kutengeneza taka hadi hatua ya mwisho ya kutupa taka ambayo ina lengo la kupunguza athali za taka kwa afya na mazingira. Mifumo hii hujumuisha tangu ukusanyaji, usafirishaji, kuzitibu na kuzitupa. Mifumo hii ni ya kitaalamu japo mingine tunaifahamu na tunaitumia katika maeneo yetu. Lengo la kudhibiti taka ni kupunguza athari mbaya za taka kwa afya na mazingira.

Leo tutazungumzia hatua za msingi katika kukabiliana na takataka katika makazi yetu. Hatua hizi ni za msingi katika maeneo yote yale ambayo huhusika na kudhibiti taka, japo sisi tutazitazama katika mazingira ya nyumbani.

JIZUIE NA PUNGUZA KETENGENEZA TAKA

Hapa tunazungumzia kupunguza kiasi cha ujazo wa takataka zinazotengenezwa bila kuongeza athali ya taka zinazotengenezwa. Hii inasaidai kupunguza kiasi cha athali kwa afya na mazingira. Kitaalamu shughuli yeyote ya awali kabla ya kutengeneza taka, ambayo itakusaidia kupunguza ujazo wa takataka bila kuongeza athali ya taka inahusika katika kipengere hiki. Baadhi ya hatua unazoweza kuchukua nyumbani ni

Kwa kufuata hatua hizi unaweza kupunguza asilimia kubwa ya taka unazotengeneza pale nyumbani kwako. Kipengere hiki unaweza kukijumuisha tangu katika ujenzi wa nyumba yako; Mfano, nunua kiasi kinachohitajika tu cha vifaa vya ujenzi kama vile rangi, mbao, saruji n.k. Pia ununuaji wa vifaa vile ambavyo ni bora na ambavyo vinadumu kwa muda mrefu. Badala ya kununua rangi kwenye makopo ya lita 4, basi nunua katika ndoo za lita 20.

ZIPE TAKA MATUMIZI MBADALA

Awali katika tafsiri ya taka nilielezea kwamba takataka sio taka, bali ni taka kwasababu huyo mtu hazihitaji, kwa hiyo bado zina thamani kwa mwingine. Kipengere hiki kinahamasisha kutambua thamani ya taka ulizonazo na kuzipa matumizi mbadala ambayo yataleta faida.

Tukianza na maji-taka; jaribu kuyapa maji-taka matumizi mbadala. Hii inaanza tangu bafuni kwenda jikoni hadi nje uani.

Maji yaliyotumika kuoshea matunda na mbogamboga yanaweza kutumika kumwagilia bustani. Maji yaliyotumika kufulia huweza kutumika kudeki na kusafisha choo.

Uvunaji wa maji ya mvua hujumuisha pia yale maji ambayo humwagika katika sehemu za wazi kama vile paving blocks na nyua; maji haya yanapokusanywa huweza kutumika kwa umwagiliaji n.k. Ni muhimu kuwasiliana na wataalamu kukutengenezea mfumo ambao umekaa makini utakaodumu.

 

Taka ngumu zaweza kutumika kwa matumizi mbadala mengi, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba zinatumika bila kuwa na sumu.

Kwa ujumla, twaweza kubadili takataka kuwa na matumizi mengine, cha msingi ni kutambua uwezo wa hiyo taka katika kukusaidia katika mahitaji yako mbalimbali.

BADILI TAKA KUWA BIDHAA ITAKAYO KUFAA NA KUTENGENEZA NISHATI

Kuna baadhi ya taka zinaweza kubadilishwa katika mazingira ya nyumbani kuwa bidhaa yenye tija; lakini kuna baadhi ya taka kama vile plastiki zinahitaji mazingira ya kiwanda ili kubadilishwa.

Nishati inaweza kutengenezwa kutoka katika baadhi ya taka, hivyo huweza kusaidia kupunguza kiasi cha takataka pamoja na kuleta tija ya kinishati. Kutengeneza nishati kutokana na taka  mara nyingi kumekuwa kukisaidia pia kupunguza athali ya taka kwa mazingira na afya.

TUPA TAKATAKA

Hii ni hatua ambayo ni ya mwisho katika kudhibiti taka. Utupaji taka ufanyike baada ya taratibu nyingine za kudhibiti taka kufanyika ikiwa ina maana ya kwamba iwe kwa namna fulani kabisa mmeona hamuwezi kuzitumia tena hizo taka. Utupaji taka uwe ni hatua ambayo imeonekana kabisa kwamba kutupa taka ni faida kabisa kuliko kubaki nazo. Swala la kutupa takataka linapaswa kufanyika katika uangalifu ili lihifadhi mazingira na afya. Utupaji taka hujumuisha maji-taka na taka-ngumu.

Mwisho katika maada yetu ya kudhibiti taka katika nyumba zetu, ni muhimu kukumbuka kuwa taka sio taka ikimaanisha kwamba waweza kuzitumia taka kwa manufaa zaidi. Taka zimekuwa taka kwasababu mtu huyo ameona hazimfai kwa muda huo, ijapokuwa mwingine zinaweza kuwa kitu chenye thamani kwake. Ni muhimu udhibiti taka ufanyike katika utashi wa kulinda afya na kuhifadhi mazingira. Jaribu kuzipa taka matumizi mbadala yenye tija kwako, na swala la kuzitupa liwe la mwisho kabisa. Wapo wataalamu wengi katika nchi yetu ambao wanaweza kukupa huduma ya kuwa na mfumo mzuri katika nyumba yako wa kudhibiti taka, kinacho hitajika ni nia ya dhati.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *