Siku zote inahitajika ujuzi na makusudi ya dhati ili uweze kupata kazi au tenda za ujenzi kwa idadi ile unayoitaka. Kazi hutafutwa kwa maamuzi na sio kutegemea zije zenyewe bila jitihada. Ili upate kazi basi unapaswa ufanye kazi fulani ili uweze kupata kazi unayoitafuta. Unaweza ukawa na ujuzi na kipaji kizuri katika fani yako uliyonayo lakini pale ambapo fani yako haipati soko zuri basi hali hiyo inaweza kukukatisha tamaa na ukashuka moyo katika kuendelea kukua katika fani hiyo.
Ni muhimu kuweza kujifunza kanuni kadhaa ambazo zinaweza kukusaidia ili nawe uweze kumudu njia za kuweza kupata kazi kwa urahisi. Ujenzi ni taaluma na sio ubabaishaji nikiwa na maana ya kwamba unahitaji kuanzia sasa kuweka taratibu za kujifunza taaluma hii katika Nyanja mbalimbali zinazokuhusu. Yafuatayo ni mambo 3 kati ya mengi ambayo ukiyafuata yatakusaidia uweze kujua misingi muhimu ambayo itakusaidia uweze kupata kazi kwa urahisi kwa idadi unayokusudia.
Ubora
Swala la ubora ni muhimu kwanza kabisa kabla ya mambo mengine. Ubora tunaouzungumzia hapa ni ule unaohusu uimara wa kazi, finishing nzuri, mkono mzuri wa kazi, kiwango bora kinachotakiwa, kudumu kwa kazi, kupendeza kwa kazi, ubunifu katika kazi zako na ubora ule unaopitiliza matarajio ya mteja wako na akabaki anafurahia kazi uliyomfanyia. Swala la ubora ni pana sana.
Utawezaje kufanya hivi? Hapa ni papana kidogo lakini nitakuelezea kwa ufupi namna ya kuweza kufikia hatua hii.
Kwanza unapaswa ujue kazi gani ambayo unaipenda na ipo ndani yako; kwa lugha nyingine kipaji chako ni kipi? Wewe ni mzuri katika mambo ya aina gani? Unapenda kufanya kitu gani? Watu pia wamekuwa wakikusifia katika aina gani ya kazi? Unapaswa kuenea na kushamili katika kazi ile ambayo ni kipaji chako na ambayo unaipenda kuifanya. Ukiweza kufanya hivyo basi itakusaidia kutumia nguvu kidogo kuifanya kazi hiyo vyema sana lakini pia inakuwa ni rahisi kwako kujifunza mambo yanayohusu kazi yako kwa urahisi. Ukifanya hivi itakusaidia pia kuwa mvumbuzi na mbunifu katika kazi hiyo na uweze kushamili sana.
Nakubali kuwa mara nyingine katika majukumu na maisha mtu unajikuta unaifanya kazi ambayo sio kipaji chako au ambayo huipendi; lakini mwisho wa siku hakikisha unafanya kazi ile ambayo unaipenda; hakikisha kufanya kwako kazi kunakuwa kwa kupenda na unajivunia kwa kazi yako kuwa bora! Hakikisha kazi yako inabeba alama sahihi ya uzuri kuhusu wewe nikimaanisha kuwa kazi yako ni alama yako uliyoiacha. Hakikisha unajiwekea ratiba ya kujifunza na kujipanua kitaaluma katika kazi yako!
Network
Network ni neno la kiingereza ambalo lina maana ya mtandao. Kama mtaalamu unapaswa kujijengea mtandao imara wa kazi. Unapaswa uwe katika namna ambayo watu wanakufahamu unahusika na nini na unafanya nini haswa specifically. Unapaswa uwe katika sehemu ambayo pale kazi na fursa zinazohusiana na mambo ya ujenzi zinapokuja basi nawe zikupate (fursa za kazi huja mara nyingi katika mtandao wa kazi husika). Mtandao wako unapokuwa mkubwa basi chance yako ya kupata kazi nayo huwa kubwa. Mtandao wako unapokuwa umeenea maeneo mbalimbali, basi ni rahisi pia kwa wewe kuweza kupata kazi kutoka maeneo mbalimbali.
Zipo namna kadha za wewe kujenga mtandao utakaokusaidia kuweza kupata kazi zako kwa urahisi. Njia moja wapo ni kufahamiana na kujenga mahusiano mazuri na wale watu wenye maamuzi ya kazi fulani ifanyike ili siku wanapotoa maamuzi ya kazi fulani kufanyika basi na wewe uwepo katika mlolongo watakaoipata. Unaweza pia kujiunga na vikundi mbalimbali vya watu wanaofanya kazi za mtindo huo husika ili muweze kujuzana fursa na changamoto mbalimbali zinapotokea. Pia unashauriwa uwe na business cards za kuwaachia watu fulani muhimu ili wasikose mawasiliano na taarifa zako za kikazi.
Katika mtandao wetu wa Makazi tunaruhusu wataalamu mbalimbali wa mambo ya ujenzi kuweza kujisajiri bure na kuziweka taarifa zao za kazi za ujenzi mtandaoni ili mtu fulani anapotafuta mtaalamu wa aina fulani basi aweze kukupata. Ni muhimu kujisajiri katika mtandao huu kwa sababu miaka ya siku hizi yule ambaye hajajiunga na mfumo wa mtandao (internet) anakua mara nyingi amejitenga na fursa nyingi za kiuchumi. Ziweke mara kwa mara kila siku taarifa na kazi zako katika mtandao wako wa Makazi ili ikusaidie kuunganishwa na wateja kibao kutoka mikoa yote Tanzania na nje ya nchi.
Huduma kwa mteja
Huduma kwa mteja ni jambo la muhimu sana pale ambapo unataka kuwateka wateja. Wateja wanahitaji namna ya kuweza kuwamudu ili uweze kuendana nao. Bila kujali hali ya mteja na hadhi yake, mteja yeyote ni mfalme na chochote ambacho mteja anakisema au kukitaka hutakiwi kumkosoa bali unatakiwa ujue namna ya kuweza kumjibu na kumshauri vyema.
Kazi yeyote ambayo unaifanya ya mteja basi hakikisha umemkabidhi akiwa ameridhika na kuifurahia. Hakikisha mteja wako pale ambapo anafikiria kuhusu kazi fulani basi wewe uwe mtaalamu wa kwanza kukutafuta kwajili ya kazi hiyo. Mteja anapofanya kazi na wewe anapaswa ajisikie raha, usalama na kuridhika zaidi ya alivyotarajia.
Huduma kwa mteja haiishii katika kuifanya kazi tu, ila inakwenda hata baada ya kukabidhi kazi yako. Hakikisha unajijengea tabia na ratiba ya kutembelea kazi mbalimbali ambazo umeshawahi kuzifanya kwa wateja wako. Jitahidi uwe unajua mrejesho wa kazi ambazo umekabidhi miaka kadhaa iliyopita. Kwa zile kazi zilizopata hitirafu jitahidi kuangalia namna ya kufanya marekebisho kwa bure au ofa kama unaweza.
Kwa njia hii basi wateja wako watakuwa wamepata msaada mzuri katika mambo yao na wataweza kuwajulisha wengine kuhusiana na wewe. Siku zote binadamu hutafuta kwanza uhakika na usalama wa huduma au kitu fulani anachotaka kukinunua; uhakika na usalama hujengwa kwa kufahamiana na mahusiano mazuri. Hakikisha unajenga mahusiano mazuri ya kikazi na wateja wako yenye nidhamu na heshima na yasiyoleta nia ovu au kuleta mashaka kwa aina yeyote. Hakikisha pia unahifadhi mawasiliano ya wateja wako vyema siku zote.
Kama ambavyo nimeeleza kwa ufupi kuhusu namna ya kufanya ili uweze kupata kazi nyingi kwa urahisi zaidi, basi ni muhimu kuhakikisha unachukua hatua zaidi katika kujifanya bora katika kazi zako. Siku zote akili yako inapaswa kujikita katika kuhakikisha unampatia mteja wako kitu ambacho kitamfurahisha zaidi ya alivyofikiria. Hiyo iende sambamba na kuweka juhudi katika mtandao wa kupata kazi ili ajira yako iwe yenye tija na usikatishwe na tamaa. Jiunge sasakatika mtandao wa Makazi kama njia mojawapo ya kujiongezea network ya kazi kutoka mikoa yote Tanzania na nje ya nchi.
Tupe maoni yako hapa chini namna mtandao inavyokusaidia kupata kazi!