Swala la ujenzi ni moja kati ya maswala nyeti ambayo yanayowafikirisha watu, taasisi na serikali namna ya kutekeleza. Kiasi kikubwa cha fedha hulipwa ili kuendesha ujenzi. Asilimia kubwa ya uwekezaji kwa watu na taasisiunalenga katika ujenzi. Hata serikali hutumia asilimia kubwa ya bajeti katika ujenzi. Serikali, taasisi, makanisa huwekeza katika ujenzi kwa gharama kubwa. Ni muhimu sana kuwa makini katika swala hili kwani ni vyema kuwekeza nguvu zako katika sehemu iliyo sahihi. Itakuwa jambo la kuumiza pale ambapo ukajenga nyumba ambayo haita kufaa.
Swala la ujenzi linahitaji utaalamu wa kutosha tangu katika kuandaa wazo, kusanifu jengo hadi katika kujenga. Wataalamu wa ujenzi hutumia hadi zaidi ya miaka 5 kusomea ujenzi ili tu kuhakikisha ujenzi unafanyika katika ubora wake.
Zipo aina nyingi za nyumba kutegemea bei, mwonekano, kimo, vifaa vya ujenzi, mitindo n.k. Inahitaji umakini na uangalifu mkubwa katika kuchagua nyumba ambayo itakufaa ili kuwekeza nguvu zako katika sehemu sahihi. Ni hasara kugharimia kitu ambacho hakitakufaa, tena kugharimia kwa gharama kubwa ya mamilioni. Ni hatari kuchukua ramani yeyote ile na kujenga.
Mambo ya muhimu katika uchaguzi wa nyumba ya kujenga
Jenga nyumba itakayokidhi mahitaji yako
Mahitaji yanaweza kutofautiona kutoka mtu na mtu, eneo na eneo. Nyumba ambayo anajenga kijana inaweza kutofautiana na nyumba ambayo atajenga mzee. Nyumba itakayojengwa Iringa itakuwa na utofauti na ile ya Pwani.
Ni muhimu kuchanganua mahitaji yako katika hali ya muda wa sasa na wa baadae. Je, ukiwa mzee itakufaa? Pia hiyo nyumba ni ya muda mfupi tu au ndio dream house?
Tazama pia mahitaji ya watumiaji katika nyumba hiyo; kama vile kuna walemavu, wazee, watoto. Ni muhimu kuwa na nyumba ambayo watoto wanaifurahia (sehemu za michezo, usalama). Kumbuka makundi maalumu.
Fikiri kuhusu gari, wanyama wa kufugwa, wageni, hali ya hewa, usalama, baadaye utakapo kuwa umezeeka, ukubwa wa eneo la ardhi, jirani zako, afya zenu, utulivu, kujisomea, maombi, ibada. Kumbuka pia kuhusu ndoa yenu, chumba cha baba na mama.
Wakala wa mteja (client agent) na Msanifu wa majengo (architect) wataweza kukusaidia katika kuchanganua mahitaji yako.
Jenga nyumba inayoafiki sheria na taratibu za ujenzi za eneo
Ni vyema kutambua eneo ulipo kama lina sheria gani ambazo zinaathiri ujenzi wako? Je upo eneo lililo pimwa kisheria? Upo jirani na vyanzo vya maji? Je upo jirani na hifadhi ya barabara? Je eneo hilo lina ruhusiwa kujengwa ghorofa ngapi?
Pia ni muhimu kufuata taratibu zinazopaswa katika ujenzi. Serikali inahitaji taratibu gani utekeleze ili kukuruhusu kujenga? Ghorofa unalotaka kujenga limekamilisha michoro yote ya ujenzi?
Ni muhimu kufuata taratibu na sheria zote ili kwenda na ujenzi wako bila bugudha. Je, watu ambao wanahusika na ujenzi wako wanaruhusiwa kisheria? Je, nyenzo za ujenzi unazotumia zinakubarika kisheria? Ni halali? Ni vyema kuhifadhi risiti.
Jenga nyumba yenye usalama
Swala la usalama ni swala la lazima. Usalama unaanza tangu katika ujenzi, utumiaji hadi ubomoaji. Usalama lazima uzingatie mtumiaji wa nyumba na asiye mtumiaji wa nyumba. Nyumba inayotililiza maji machafu kwa jirani haina usalama wa kutosha. Usalama unalenga toka kizazi cha sasa hadi cha baadae. Usalama toka katika mwili hadi akili.
Nyumba inapaswa iweze kuhimili na kukinga nguvu mbalimbali zinazoweza leta hatari kama upepo, tetemeko, uzito wa jengo lenyewe, milipuko, moto. Paa lililotengenezwa vibaya linaweza leta hatari kubwa pale upepo mkali utakapo vuma. Nyumba iliyokosa msingi imara inaweza kushindwa kuzuia nyufa mbalimbali zinazoweza kuipiga. Nzege yenye saruji chache inaweza kuleta mipasuko na kuanguka. Nguzo, kuta, slabu, mihimili, paa, msingi vina mchango mkubwa sana katika kuhimili nguvu mbalimbali zinazoweza kuipiga nyumba.
Uwepo wa choo, mifumo ya kudhibiti takataka, sehemu ya kuhifadhi vitu, mzunguko mzuri wa hewa, vifaa visivyo na sumu huchangia kuboresha afya ya viumbe hai wanaohusika na mazingira ya jengo. Nyenzo zenye sumu huweza kuchangia matatizo ya uzazi. Ni muhimu kupunguza utengenezaji wa taka katika eneo lako. Je, nyumbani kwako unadhibiti vipi taka?
Usalama wa nyumba katika wezi na wanyama wakali nalo ni muhimu. Hii inategemea na eneo na utamaduni wako. Ni muhimu kuweza kujua kiasi gani cha ulinzi ukiweke ili kuepuka vibaka, majambazi na wanyama wasio hitajika. Nyumba yako pia inapaswa iwe na mazingira ya faragha kwa kiasi kinachoridhisha. Swala la faragha hutegemea mtu na mtu. Chumba cha baba na mama, cha kusomea, cha maombi ni vyema viwe katika mazingira yenye faragha ya kutosha.
Usalama uzingatie wakati wa sasa na wa baadaye, uzingatie vizazi vya sasa na vya baadaye. Usalama pia ujali uwepo wa makundi maalumu kama watoto, wazee, walemavu. Ujenzi wa nyumba uzingatie usalama wa eneo lako na mazingira ya ujumla. Ujenzi wa nyumba katika maeneo yaliyokatazwa na mamlaka husika si salama.
Jenga nyumba iliyo imara na yenye kudumu
Uimara wa nyumba unakuhakikishia nyumba yako kuwa itaweza kuhimili nguvu, pepo, mvua, uzito wote utakao ipiga. Mara nyingi kwa nyumba za kawaida uimara upo katika msingi, kuta, paa, nguzo, mihimili. Pia milango, madirisha, dari n.k. Japo kuwa ni mambo ya kitaalamu zaidi, lakini ni vizuri kufuatilia yanafuatwa ili kuepuka uharibifu na ajali mbalimbali. Ni muhimu kununua tofali na nyenzo nyingine za ujenzi zilizo katika ubora wake. Epuka uchakachuaji.
Ni muhimu kujenga nyumba itakayodumu kwa muda unaokufaa. Hii itakusaidia kupata maamuzi katika kuamua gharama za ujenzi. Nyumba iliyo bora ya matofali inaweza kudumu zaidi ya miaka 80. Vifaa vya ujenzi vinaweza kudumu kwa miaka 5, 15, 30 kutegemea na teknolojia. Kwanini ununue kifaa cha kudumu miaka 5 kama unataka nyumba yako idumu miaka 50?
Jenga nyumba yenye uzuri wake
Uzuri wa jengo unategemea vitu vingi. Wasanifu majengo hujitahidi kusanifu nyumba ambayo inagusa hisia za mtu. Uzuri unahusisha hisia za mguso, kuona, kunusa, ladha na harufu. Jengo lenye uzuri wake ni zaidi ya kuathiri hisia za kuona.
Majengo yenye mwonekano mzuri ni alama nzuri kwa eneo hilo. Uzuri wa jengo huongeza thamani ya jengo. Uzuri wa jengo huvutia watu wanaolitumia na kuwapa hisia za kitofauti. Mandhari ya jengo iliyowekwa katika uzuri wake huweza kuleta hisia za utulivu, uasilia, furaha, uchangamfu, uhuru n.k.
Ni muhimu jengo liwe na uzuri unaoendana na matumizi yake. Majengo ya biashara yawe na uzuri unaovutia wateja. Chumba cha baba na mama kiwe na uzuri wa kujenga ndoa. Chumba cha watoto kiwe kinaendana na umri wao. Chumba cha kusomea kiwe chenye kuvuta hisia za kusoma. Chumba chako cha tafakari na maombi kinajenga hisia gani unapoomba?
Rangi, mwanga, unyororo, mpangilio, mpishano, kimo, mfanano, ukubwa, umbile la nyumba yako huathiri hisia za mtumiaji. Rangi nyeupe huweza leta hisia za usafi, utaratibu na amani. Kijani huweza leta hisia za utulivu, uasilia, amani. Nyekundu huweza leta hisia za kusisimua, shauku, changamfu. Rangi waridi huweza leta hisia za furaha. Bluu huweza leta hisia za uasilia, utulivu, n.k
Usanifu wa nyumba unahusisha jengo lenyewe, mazingira ya ndani, mandhari ya nje ili yabebe maana fulani. Uzuri wa jengo hubeba maana fulani ambayo mtu huweza kuisoma hiyo maana na kujua mlichomwabia. Ni muhimu kuwa makini na maana unayomwambia mtu kupitia nyumba yako.
Jenga nyumba utakayoweza kumudu gharama zake
Swala zima la gharama linaweza kugawanyika katika vipengere viwili; gharama za ujenzi na gharama za kuiendesha nyumba. Swala la gharama linaanza tangu ununuaji wa kiwanja, kuandaa michoro na taarifa za kitaalamu, ujenzi, usimamizi wa mradi hadi uendeshaji wa jengo. Ulipaji wa gharama ni muhimu ili kupata kitu au huduma fulani unayoihitaji. Gharama utakayolipia kupata dhahabu ni tofauti na gharama utakayolipia kupata chuma. Jifunze kulipia gharama, usitegemee kupata kitu kizuri bila kulipia gharama inayostahili. Gharama inaweza kuwa nguvu zako, kubadilishana mali,fedha, mahusiano na vingine vingi.
(Luka 14:28-30 BHN)Kwa maana, ni nani miongoni mwenu ambaye akitaka kujenga mnara hataketi kwanza akadirie gharama zake ili ajue kama ana kiasi cha kutosha cha kumalizia? La sivyo, baada ya kuweka msingi na kushindwa kumaliza, watu watamcheka wakisema: ‘Mtu huyu alianza kujenga, lakini hakumalizia.’
Ni muhimu kujua makadirio ya gharama za ujenzi kabla ya kuanza ujenzi wako.Makadirio mazuri hufanyika kitaalamu katika mchanganuo mzuri.Faida zake ni:-
- Hukusaidia kujua gharama utakazohitaji kulipia mpaka kumaliza ujenzi wako.
- Kujua utahitaji gharama kiasi gani kujenga toka hatua moja hadi nyingine
- Kujua aina, kiasi na gharama za vifaa vya ujenzi utakavyohitaji; ili upange wapi pa kwenda kuvipata na ununue kwa mfumo gani
- Hukusaidia katika kujadiliana na kupatanajuu ya bei ya ufundi na vifaa vya ujenzi
- Hukusaidia katika kufanya mchanganuo ili kukuwezesha kufanya maamuzi vipi vya kufanya na kutofanya, vipi vya kubadili, kuongeza au kupunguza n.k.
- Hukuwezesha kujua na kudhibiti wizi, upotevu na uvujaji wa vifaa vya ujenzi pindi ujenzi wako unapoendelea
Tambua uwezo wako wa mwisho utakaoweza kujitoa kulipia hizo gharama. Je, hiyo gharama utaweza kuimudu? Au umejikadilia kiwango kidogo? Unaweza jipanga na ukajiongeza kipato ili uweze kumudu hizo gharama. Mtaalamu utakayemchagua akuongoze katika ujenzi au kusanifu jengo lako, unaweza mshirikisha swala la gharama na mkaangalia namna ya kupata nyumba bora utakayoweza kumudu gharama. Zipo njia kadhaa zinazoweza kutumika kushughulikia swala la gharama nafuu za ujenzi.
Kitu kingine cha kukumbuka katika gharama ni gharama za uendeshaji wa nyumba. Kuna watu wamejenga nyumba ambazo zinawachosha kumudu gharama za uendeshaji. Gharama za usafi, umeme, maji, wafanyakazi wa kuhudumia bustani n.k. Pia gharama za kudumisha na ukarabati wa nyumba. Hata kama pesa ipo ni muhimu kupunguza gharama za uendeshaji kwani husaidia kuokoa mazingira, kutoshereza rasilimali zilizopo kwa wote. Fikiri juu ya umeme wa jua, madirisha yenye hewa na mwanga wa kutosha, kuvuna maji ya mvua, maji ya visima, kupunguza taka na kuzipa matumizi mbadala, taa zinazojizima zenyewe.
Mwisho wa mada yetu ya kufafanua aina ya nyumba inayokufaa kujenga, ni muhimu kukumbuka kuwa asilimia kubwa ya muda wetu tunatumia tukiwa maeneo ya nyumba, nyumba inabeba ujumbe wa kuwaambia watu, nyumba huathiri biolojia yetu, nyumba hugharimu gharama kubwa.
Jambo la msingi kukumbuka, ni vyema kujenga nyumba ile unayoihitaji; itakayokidhi mahitaji yenu ya sasa na ya baadaye. Usalama na uimara wa nyumba ni lazima. Nyumba iliyo katika uzuri wake huridhisha, huvutia na ni alama nzuri kwa jamii. Usijenge nyumba ya majivuno, usiyo ihitaji. Kumbuka kufuata sheria za ujenzi na taratibu za kitaalamu za ujenzi.