MAMBO AMBAYO WANAWAKE HUYAJALI NA AMBAYO HAWAYAJALI SANA KATIKA UJENZI WA NYUMBA

Katika miaka kadha ambapo nimekuwa nikiandaa miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba za kuishi, moja ya vitu ambavyo nimevigundua ni nafasi ya mwanamke katika ujenzi wa nyumba. Wanawake wamekuwa na mtizamo na mapendeleo tofauti katika ujenzi wa nyumba tofauti na wanaume. Katika familia ambayo kuna mume na mke, utofauti ni rahisi sana kuonekana katika mitazamo yao.

Jambo la kwanza mwanamke hutaka nyumba zaidi kuliko mwanaume. Katika miradi mingi ambayo nimeiandaa, mtu wa kwanza kuleta wazo la kujenga nyumba ni mwanamke; mke alianzisha wazo na akamshawishi mume katika kulitekeleza. Uhitaji wa kuwa na nyumba ya familia kwa mwanamke ni mkubwa zaidi kuliko mwanamume. Hupendelea zaidi nyumba ambayo ni ya familia moja, yenye uhuru wa kifamilia, isiyo na usumbufu toka kwa majirani, ambayo yeye ndiye atakuwa mwenye mamlaka juu ya yote, ambayo hatapata usumbufu toka kwa mwanamke mwingine, awe na uhuru wa kufanya anavyoona yeye inafaa kuiendesha na kuimudu. Kwahiyo hupendelea kukaa kwenye nyumba ya kupanga yenye uhuru wa kifamilia zaidi, tena hupendelea sana kuwa na nyumba yao zaidi kuliko ya kupanga.

Pia katika kusanifu nyumba za kuishi, mwanamke amekuwa na mchango mkubwa katika kupendekeza nyumba iweje ambavyo yeye anaona itaweza kuifaa familia.

Wanaume wamekuwa wakiona nyumba kama vile ni kitega uchumi zaidi, sehemu ya kuiweka familia, sehemu ya kulala baada ya kutoka kazini, jengo; Lakini wanawake wamekuwa wakiona nyumba kama ni home, ufalme wao wanaomiliki, sehemu muhimu ya kuweza kuihifadhi familia, the ultimate place to live, enjoy, relax, work. Siku zote ukimpa mwanamke a house, ataibadili kuwa a home.

Mambo haya ni muhimu kuweza kujifunza ili kuweze kuwa na maamuzi sahihi katika kuanda makazi yenu ya kuishi. Pia inasaidia hata kwa wataalamu wengine kuweza kuwa makini katika kutimiza matakwa ya wateja. Mwanamke na mwanume wote ni binadamu wenye tabia na hulka tofauti ila wanaishi pamoja.

Katika maada yetu tutaangalia mambo ambayo wanawake wanayajali sana na mambo ambayo hawayatilii maanani sana. Yapo mambo ambayo ni ya muhimu Lakini wao hawayatilii maanani sana; hivyo kama mwanamume ni muhimu kuwa nayo makini.

Mambo ambayo wanayatilia maanani zaidi

Mpangilio wa vyumba

Moja kati ya mambo ambayo ni ya muhimu katika ujenzi wa jengo ni mpangilio wa vyumba. Mpangilio wa vyumba ni muhimu kwajili ya kuweza kuruhusu mtiririko mzuri wa shughuli katika jengo bila kuleta adhaa au kukwama kwama.

Wanawake wengi wamekuwa wakipenda chumba cha baba na mama kiwe kimejitenga pembeni kabisa ya nyumba penye usiri; kiwe kimekaa jirani na vyumba vya watoto (hasa kama watoto ni wadogo) kwa maangalizi zaidi. Pia hupendelea vyumba vya watoto na wazazi vikae sehemu iliyo nzuri zaidi kuliko vingine. Hupenda sebure iwe imekaa mbali na vyumba; sebule iwe imekaa katika upande mzuri wa kukalibisha wageni; mtu wa sebureni asione jikoni. Wengi hupendelea jiko, stoo, na vyoo viwe ‘vimejificha’ mbali na sehemu za wageni. Wengi hutaka sana kibaraza cha jikoni kikubwa, jiko la nje na stoo ya nje. Upande wa nyuma wa nyumba hupendelea kuwa sehemu ya shughuli nyingine kama kufua, kuongelea na marafiki zao n.k.

katika nchi yetu, wengi hupendelea mpangilio huu japokuwa wengine hupendelea tofauti kidogo kutokana na tamaduni za nje na hulka. Mpangilio wao hutokana na ni shughuli gani wanataka ziwe zinafanyika upande wa mbele, nyuma na jikoni. Mpangilio wao umejikita zaidi katika swala la usiri wa unyumba, ujirani wa watoto hasa wadogo, mkaribisho wa wageni, kukinga shughuli za nyumba zisionekane.

Wengi wamekuwa wakionesha kutilia maanani zaidi katika vyumba vya watoto na cha wazazi zaidi kuliko cha wageni. Vyumba kama vya kusomea, ofisi, cha kutazamia luninga vimekuwa vikipewa mapendekezo sio makubwa sana. Vyumba kama stoo na vyoo kwao ni vya muhimu na vina uzito tu mkubwa. Mabanda ya nje labda ya kufugia hupendelewa na baadhi kama wanapendelea shughuli hizo.

Mwonekano wa ndani

Wanawake wengi hutilia maanani zaidi mwonekano wa ndani wa nyumba kuliko wa nje. Swala la rangi limekuwa ni la muhimu kwao. Kwa wale ambao wanafahamu maswala ya kuchanganya rangi kulingana na radha wanayotaka wamekuwa wakifanya kwa ubora zaidi; rangi zile ambazo zinaendana na shughuli za chumba hicho.

Hupendelea zaidi urembo ukutani, sakafuni na darini; katika swala la marumaru za sakafuni tena zile zinazo ng’aa zaidi; kuta zilizoundwa katika mwonekano mzuri. Uwekaji wa maua katika gypsum, utumiaji wa madirisha yenye urembo fulani, miimo ya milango na milango yenye urembo.

Pia hupenda utumiaji wa maua, midori, taa na samani zenye urembo. Hawapendi pazia tu, bali pazia lenye ladha nzuri ya kipekee. Namna makabati yanavyopangwa na kuonekana. Kwa ujumla mpangilio wa samani na mwonekano wake wa samani kwa ujumla hupendelea uwe wenye kuleta urembo wakiutofauti. Mwonekano katika chumba cha baba na mama na utumiaji wa vifaa vya kisasa vyema uzuri katika bafu lao pia hupewa kipaumbele zaidi.

Kwa lugha fupi tungesema, hupendelea mwonekano wa ndani uwe wa kiurembo zaidi, wenye kuleta mshangao mzuri kwa mgeni, wenye kuvutia watumiaji. Urembo huanzia sebureni, chumba cha kulia chakula, chumba cha baba na mama mpaka chooni. Hupendelea ndani kuwe kuna harufu na mwonekano wenye kuvutia zaidi. Wengi hupenda kubadili mwonekano mara kwa mara. Kuiga mitindo tofauti tofauti na kuiga majirani.

Ukubwa wa vyumba

Kama tulivyoona kwamba wanawake na wanaume wanahulka tofauti katika maisha kwa ujumla, mapendeleo yao huweza kutofautiana. Katika swala la ukubwa wa vyumba, wanawake wamekuwa wakionesha kutaka nafasi zaidi kuliko wanaume. Ukubwa huu umekuwa kwajili ya kuweza kupata nafasi zaidi ya kuweka vitu mbalimbali walivyonavyo. Hili linafahamika kuwa wanawake wamekuwa ni watu wa kuwa na vitu vingi zaidi ya wanaume; idadi ya nguo, vyombo n.k ni kubwa. Wanawake wamekuwa wakipenda kuwa na vitu kadha ambavyo wanabadilisha kulingana na muda na majira. Wanawake huweza kubeba mikoba zaidi ya miwili katika safari zao.

Nafasi hii pia hupendelewa kwajili ya kujinafasi na kupumzika. Nafasi hii huwasaidia zaidi katika kuvipanga vitu kulingana na wao wanavyoona inawafaa; pia kupata nafasi itakayowawezesha kubadili mpangilio na mitindo kulingana na muda. Hupendelea samani za nyumbani zipangwe zikitawala vyema ujazo wa chumba huku zikileta muonekano wenye ladha nzuri.

Wanawake huweza kuhitaji nyumba iwe na vyumba kwajili ya kufanyia shughuli mbalimbali. Uwepo wa chumba cha kufulia na kuhifadhi nguo, sebure ya baba na mama, sehemu ya watoto kucheza, stoo kwajili ya jiko, choo na stoo za nje n.k. hupendelea nyumbani pawe pamejitoshereza penye utaratibu mzuri kulingana na shughuli mbalimbali.

Ukubwa wa nyumba unavyoongezeka ndivyo na gharama ya ujenzi na matunzo yake nayo yanaongezeka. Ni muhimu kama familia muweze kuangalia ukubwa gani wa nyumba unawafaa na ambao mtaweza kujivuta kulipa gharama yake. Ni muhimu kuwa na nyumba yenye nafasi ya kutosha huku pia mkitazama siku za mbele; ni muhimu pia kuzitumia nafasi za wima za ukuta na makabati ya ukutani ili kuweza kuokoa nafasi katika mtazamo wa kiuchumi.

Afya

Afya kwa mwanamke ina kipaumbele kikubwa kwani yeye ndiye anayehusika zaidi katika kuhakikisha kuwa familia nzima inashamiri. Swala la afya kwa mwanamke ni kitu asilia ndani yake. Afya kwa mwanamke huanzia katika vyoo, jikoni, sehemu za kulala mpaka mazingira ya nje. Afya katika familia ikiwa mbovu mwanamke ndiye mwenye kuathirika zaidi na pia mwenye kuangaliwa zaidi.

Uwepo wa mfumo wa kudhibiti taka ni muhimu kwa mwanamke. Taka za chooni, jikoni na mazingira ya nje huangukia zaid kwa mwanamkei katika kuzitupa; hivyo hupendelea kuwe na mfumo ambao utampatia urahisi namna ya kuzidhibiti takataka hizo. Mara nyingi ukikuta kuna utupaji wa taka ovyo katika nyumba, wanaofanya kitendo hicho ni wanawake wa mazingira hayo; sababu ambayo imewafanya kutupa ni kutaka kutokaa nazo, Lakini kutokana kutokuwa na mfumo mzuri wa kudhibiti taka basi huzitupa ovyo. Ni muhimu nyumba yenu iwe na mifumo mizuri kwajili ya kudhibiti taka ili kuhakikisha kuwa panakuwa ni sehemu nzuri ya kiafya.

Afya kwa mwanamke ipo pia katika kuhakikisha kuwa mpangilio wa vyumba na nyumba kwa ujumla ni wenye kuleta ujumla wa afya. Mpangilio wa vyoo, jiko, stoo, vyumba uwe umekaa katika kuleta jumla kubwa kabisa ya afya ya familia. Kipaumbele cha afya huanzia zaidi kwa watoto na kwenda kwa wengine. Pia upo katika kuhifadhi vyakula, uhifadhi wa vyombo na vitu mbalimbali. Swala la afya lipo pia katika kuhakikisha kuwa mbu na wadudu wengine hawaleti shida katika familia. Afya kwa mwanamke ipo pia katika kuhakikisha kuwa nyumbani panavutia na kufurahika.

Uzuri

Uzuri kwa mwanamke ni kitu cha asili zaidi kwake. Uzuri hupewa kipaumbele zaidi; uzuri huamsha hisia za mwanamke; uzuri huweza kumsukuma mwanamke katika kupata kitu fulani. Wanawake wamekuwa tayari kulipia gharama hata kama ni kubwa ili tu kupata kitu fulani ambacho wamekipenda.

Katika ujenzi, wanawake wamekuwa wakisukumwa katika ujumla wa uzuri wa nyumba hasa wakianzia katika mwonekano wa ndani kwenda hadi katika mazingira ya nje. Wanawake wapo tayari kulipia gharama ili mradi tu nyumba ipendeze. Utumiaji wa samani, maua, mapazia, urembo katika kuta n.k hupewa kipaumbele. Uwepo wa bustani za nje za maua na utengenezaji wa mazingira ya nje ya nyumba ni muhimu katika kuhakikisha nyumba inavutia. Nyumba inayopendeza kwa mwanamke ni chaguo lanye nguvu zaidi ya gharama.

Ukarabati na uboreshaji wa nyumba ili iwe inavuitia zaidi hupewa kipaumbele zaidi kwa mwanamke; nyumba zilizojengwa kwa mitindo ya kizamani na zilizochakaa huboreshwa na kuwekwa urembo ili kuzifanya zivutie zaidi; upakaji wa rangi, uwekaji marumaru, ubadirishaji samani na urembo mbalimbali ni baadhi ya hatua ambazo huchukuliwa nao ili kuiboresha nyumba zaidi.

Usiri

Usiri na faragha ni jambo la muhimu katika makazi ili kuwapa watumiaji uhuru zaidi na katika kujenga jamii husika. Kiwango cha usiri kwa siku hizi kimepungua ukilinganisha na miaka ya nyuma. Madirisha yamekuwa makubwa yenye kuonesha shughuli za ndani ya nyumba, mpangilio wa vyumba umebadirika kiasi ambapo jikoni na sebureni panaweza pakawa pana mwingiliano wa kishughuli. Upunguaji wa usiri katika nyumba umetokana na mwingiliano wa kimitindo na tamaduni; Lakini pia hutokana na katika kupunguza gharama za ujenzi.

Swala zima la usiri kwa mwanamke lina kipaumbele kwani wao huhitaji kufanya baadhi ya shughuli katika usiri zaidi. Kuwepo na mtengano kati ya shughuli za jikoni na sebureni kwa wengi ni wa muhimu katika kuhakikisha faragha. Ijapokuwa baadhi ya watu hupendelea kuwepo na mwonekano wa moja kwa moja kati ya sebure na jikoni kupitia sehemu ya kulia chakula. Wengi wanapendelea jikoni na kibaraza chake pawe sehemu yenye usiri kiasi kutoka mbele ya nyumba kwa wao kuweza kuongea.

Swala la faragha lipo pia katika kuhakikisha shughuli za bafuni na vyooni zimejitenga na kupewa usiri mkubwa. Katika nyumba zetu za Kitanzania maeneo ya nyuma ya nyumba yamekuwa yakitumika kwajili ya shughuli mbalimbali kama kufua, kufuga n.k; wengi wamekuwa wakipendelea kuwe na mtengano kati ya nyuma na mbele ya nyumba. Maeneo ya kuhifadhi vitu yamekuwa pia ni maeneo yenye kuhitaji usiri.

Usiri katika vyumba huanzia katika chumba cha baba na mama; kiwe kimekaa upande wa nyumba ambao hauna mwingiliano na shughuli nyingine na wenye utulivu; pia kiwe kimekaa katika mpangilio ambao unaleta usiri kutoka vyumba vingine vya ndani ya nyumba. Hupendelea chumba kiwe kimekaa katika faragha nzuri kutoka katika shughuli za nje na za ndani ya nyumba. Ni kawaida chumba cha baba na mama kuwa na bafu la kutosha humohumo ndani, Lakini pia wengi hupenda ndani ya chumba cha baba na mama kuwepo na sehemu maalumu ya kuhifadhi, kuvalia nguo na meza ya kujipambia. Chumba cha baba na mama hupendwa kiwe chenye nafasi ya kama kisebure kidogo hata kochi moja kwajili ya kupumzika; hii yote ni kuleta usiri na faragha nzuri kwa shughuli zinazofanyika chumbani. Lakini pia usiri na faragha upo katika sauti, kuziba na kuonekana kwa shughuli za ndani. Chumba hiki hupendelewa kiwe na utulivu, kikubwa, hewa, kimejitoshereza kubeba shughuli za muhimu bila kutegemea vyumba vingine. Kutokana na uchumi na gharama za ujenzi, basi hupendelea angalau kiwe chenye utulivu na kikubwa kubeba kitanda, meza, kochi na kabati huku kikiwa na bafu la ndani. Vyumba vya watoto hupendelewa viwe jirani na chumba cha wazazi Lakini viwe katika mpangilio wa kuleta faragha kwa wazazi; ujirani huu hupendelewa zaidi kama watoto ni wadogo.

Kuhifadhi

Tumeona kuwa wanawake wamekuwa ni watu wenye kuwa na vitu vingi, pia shughuli zao za nyumbani zimekuwa zikihitaji kuhusika na vitu vingi. Uwepo wa sehemu za kuhifadhi vitu ni wa muhimu kwao ili kuhakikisha usalama na mpangilio wa vitu hivyo.

Jikoni huhitaji kuwepo na stoo ya kuhifadhi vyakula na vyombo mbalimbali; kwa zile nyumba ambazo wamekuwa wakinunua vyakula vingi kwa pamoja huhitaji kuwa na stoo kubwa zaidi. Pia uwepo wa stoo za kuhifadhi vitu mbalimbali kama vya bustani, usafi na vyombo vilivyoharibika. Kuwepo na sehemu ya kufulia, kupigia pasi na kuhifadhi nguo.

Uhifadhi upo hadi katika swala zima la makabati kutoka vyumbani hadi sebureni. Makabati ya kuhifadhi vyombo, vyakula, nguo na vitu mbalimbali. Makabati mengi katika nyumba yameshikiliwa na wanawake katika kuhifadhi vitu vyao na vya familia. Ni muhimu kuwa na nyumba yenye maeneo ya kuhifadhi ya kutosha na kutumia maeneo vizuri huku tukiokoa nafasi.

Kuna baadhi ya mambo ambayo wanawake hawayatilii maanani zaidi katika ujenzi wa nyumba, ijapo kuwa kuna baadhi yao huweza kuyachukulia kwa umakini zaidi; kwa hiyo mambo haya ni kwa wanawake wengi ijapokuwa baadhi yao wanaweza kuwa na utofauti kidogo. Ukishafanikiwa kuyajua baadhi ya mambo hayo basi ikusaidie namna ya kuyatizama kwani ni ya muhimu katika ujenzi wako na yana mchango mkubwa katika ujumla wa mradi wako. Kama ni mwanamume katika familia inakupasa uwe nayo makini ili kuhakikisha usalama wa mradi wenu! Yatazame na kuyaelewa vizuri maana hayapo moja kwa moja bali yana ukweli wake; Baadhi ya mambo hayo ni

Gharama za ujenzi

Wanawake wengi wamekuwa wako radhi kulipia gharama hata kama ni kubwa ili mradi wapate kitu au huduma ambayo wao wameipenda. Anapokuwa amekipenda kitu fulani hisia zake huchangia kujitoa zaidi na kulipa gharama husika ya kitu ili akipate. Hii ni tofauti na wanaume pale ambapo wamekuwa wakikitaka kitu au huduma fulani, wao swala zima la gharama wamekuwa wakilipima zaidi na zaidi huku wakizidi kuangalia umuhimu wa kitu au huduma hiyo; kwahiyo mpaka akinunue hicho kitu anakua tayari ameshakipima sana na kuridhia.

Hii pia huja kutokana na kwamba wanawake wengi huwa hawachunguzi na kufuatilia mambo ya kiugumuugumu kama ujenzi, kwahiyo wanakuwa hawana kupima kuhusiana na uzito wa gharama hiyo. Hivyo wengi wao wamekuwa wakipokea na kuridhia gharama ambayo wanaambiwa bila kuipima vizuri. Pia pale ambapo wanapokuwa wamekumbana na ugumu katika kazi hiyo, basi wamekuwa radhi kuilipa gharama husika ili wasipate usumbufu.

Sababu nyingine ni kutokana na majukumu na hulka zao za maisha, mara nyingi mzigo wa kiuchumi wa kifamilia upo zaidi kwa baba kuliko mama. Kwa zile familia zenye baba na mama, mgawanyiko wa kimajukumu huweza kuleta utofauti wa uzito wa fedha. Siku zote mtoto huwa na mtazamo kwamba chochote ambacho atakiomba kwa baba yake atakipata; basi hata mwanamke ambaye ameolewa anaweza kuwa na aina fulani ya fikra kama hizo.

Mwonekano wa nje wa nyumba

Tumeona mwanzo ya kuwa wanawake wengi wamekuwa wakitilia maanani zaidi mwonekano wa ndani kuliko mwonekano wa nje wa nyumba. Uzuri wa nyumba kwao upo zaidi katika mwonekano wa ndani zaidi ya nje; mambo ya rangi, mpangilio wa samani, mapazia na mapambo mengine mengi huwa na uzito zaidi kuliko mwonekano wa nje wa nyumba.

Hii haimaanishi kwamba hawajali mwonekano wa nje, bali inaonesha utofauti wa uzito katika hayo mambo mawili. Katika mitandao ya kijamii picha nyingi za mwonekano wa ndani hupendwa na wanawake zaidi kuliko wanaume, wanaume wengi wamekuwa wakipenda zaidi sura ya nje ya nyumba kuliko ndani.

Mazingira ya nje ya kiwanja

Mazingira ya nje ya kiwanja yanajumuisha mifereji ya barabarani karibu na nyumba, barabara, mipaka na majirani, usalama wa kiwanja n.k. Kwa wanawake uzito wa umakini upo zaidi katika mazingira ya nje ya kiwanja kuliko ya ndani; wanawajibika na kuchukua hatua zaidi kwa mambo ya ndani ya kiwanja kuliko yale ambayo yanaendelea nje ya kiwanja chao. Wanatilia umakini zaidi katika usalama na uhifadhi kuliko ulinzi. Utofauti upo kwa wanaume ambapo wao mazingira ya nje ya kiwanja huyatazama zaidi haswa katika swala la ulinzi.

Uimara na kudumu

Swala zima la uimara na kudumu linahusiana na mambo ya uwekezaji, ulinzi, uhakika wa kazi na maswala ya baadaye. Ni swala lenye mkazo zaidi kwa mtu ambaye anaangalia kesho, anafikiri zaidi kwa miaka ijayo. Ni swala ambalo linatazamwa zaidi kwa mtu yule ambaye anatilia mkazo zaidi uwekezaji, thamani ya kitu, ulinzi na usalama wa kitu. Wanaume wamekuwa ni watu ambao wamekuwa wakitaka kazi ifanyike katika misingi ya ubora, uhakika, uwekezaji na usalama. Wanaume wamekuwa ni watu ambao wapo makini katika kuhakikisha usalama zaidi ya uzuri, thamani zaidi ya kupata kitu, kesho zaidi ya leo, uwekezaji zaidi ya kumiliki. Hii inatokana na majukumu ya wanaume kama kulinda na kutoa.

Undani wa kazi

Wanawake wengi wamekuwa hawajui sana undani wa kazi na wamekuwa hawana kiu kubwa ya kujua namna kazi inavyofanyika. Kujua mchanganuo wa gharama, idadi ya vifaa vitakavyotumika, kujua mgawanyiko wa wafanyakazi na ulipaji wake. Kujua namna kazi inavyofanyika na mbadala wake, kujua kipi kilicho fanyika leo na kipi kitakachofanyika kesho. Kujua hali na namna kazi inavyokwenda. Hii yote ni mitazamo ya kiuwekezaji ili kuhakikisha usalama, uhakika wa kazi na thamani ya kazi. Hii huonekana zaidi katika familia ambapo kuna mgawanyiko wa kimajukumu kati ya baba na mama.

Undani ambao wanawake hutilia maanani ni ule wa kuhakikisha nyumba inakuwa kama wao wanavyotaka; katika maswala ya uzuri, mwonekano, uhifadhi, mpangilio wa vyumba. Swala la kujua kazi inafanyikaje na mgawanyiko wake upoje, wao hawatilii maanani sana. Hawatilii mkazo zaidi katika kutafuta na kudadisi undani wa mambo. Wanaume ni watu wachunguzaji, wapimaji, watu wenye kufikiri na kutoa maamuzi kwa akili, watizamaji mbali na wenye msimamo thabiti. Wanaume wamekuwa wakitaka kuhakikisha kwamba mambo yote yanakwenda vyema kama wao wanavyotaka. Wanaume hupenda kusababisha mambo kutokea kama wao wanavyotaka.

Kama tulivyoona mambo ambayo wanawake huyatilia maanani zaidi na yale ambayo hawayatilii maanani zaidi, basi ni muhimu kuweza kuyatizama katika mtazamo mzuri na kuenenda nayo vyema. Jambo la muhimu katika maada yetu ni uwe umeweza kujua mtizamo na saikolojia ya wanawake na wanaume katika swala la ujenzi. Pale ambapo tunapokuwa tumeweza kujua nini watu hawa wanafikiri na kutaka, basi inatusaidia namna ya kufanya maamuzi sahihi. Katika familia, swala la kujenga ni vyema lifanyike huku baba na mama wote wakishirikiana katika kuhakikisha mradi wa ujenzi unafanyika kwa ubora zaidi huku pande zote zikifurahia.

 

mangula
Eng. Makazi Team
Makazi.ne.tz ni mtandao mahususi Afrika Mashariki wenye lengo ...
ID-18112
3
139 sqm
96 Pcs
13 m
2,488 Pcs
11 m
1,237 Pcs
ID-27291
4
208 sqm
143 Pcs
17 m
3,723 Pcs
15 m
1,851 Pcs
ID-16141
3
231 sqm
159 Pcs
19 m
4,135 Pcs
14 m
2,056 Pcs
ID-10129
3
100 sqm
33 Pcs
12 m
2,024 Pcs
10 m
890 Pcs
ID-17766
3
160 sqm
110 Pcs
14 m
2,864 Pcs
13 m
1,424 Pcs
ID-19356
3
225 sqm
92 Pcs
18 m
5,400 Pcs
17 m
2,003 Pcs
ID-16782
4
225 sqm
155 Pcs
17 m
4,028 Pcs
15 m
2,003 Pcs
ID-26453
3
135 sqm
55 Pcs
14 m
3,290 Pcs
13 m
1,202 Pcs
ID-20671
16
356 sqm
312 Pcs
29 m
6,974 Pcs
17 m
3,169 Pcs
ID-17562
4
432 sqm
149 Pcs
19 m
10,625 Pcs
14 m
2,715 Pcs
ID-16582
3
180 sqm
124 Pcs
16 m
3,222 Pcs
15 m
1,602 Pcs
ID-18092
3
224 sqm
70 Pcs
11 m
6,439 Pcs
10 m
1,709 Pcs
Makazi Icon Blue

Join Membership

Join Membership to See Clear Floor Plans Before You Buy the Full Plan; See How Much MONEY is Needed to INVEST in Your Business In order to Get the Profit to Finance Construction of This House. What MORTGAGE to Borrow and Return Monthly to Your Bank. Also, See How Much it COSTS to Build the Foundation, Walling, Roofing, Ceiling, Painting, Doors, Windows… in All of Our Houses on This Platform so That You Can CHOOSE, COMPARE, PLAN & STRATEGIES on How to Approach Your Construction Rightly!